Spika wa Bunge la Uganda ametangaza kuwa Rais Museveni ameutia saini muswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja kuwa sheria.
Spika Anita Among , amesema Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ametekeleza majukumu yake ya kikatiba kama ilivyoainishwa na Ibara ya 91 (3) (a) ya Katiba. Ameidhinisha Sheria ya Kupinga mapenzi ya jinsia moja, aliandika katika taarifa yake aliyoituma kwenye mtandao wa Twitter.
”Kama Bunge la Uganda, tumejibu kilio cha wananchi wetu. Tumetunga sheria ili kulinda utakatifu wa familia kulingana na Kifungu cha 31 cha Katiba ya Uganda”.
”Tumesimama kidete kutetea utamaduni wetu na matarajio ya watu wetu kulingana na malengo ya 19 & 24 ya malengo ya kitaifa na kanuni za maagizo ya sera ya serikali. Namshukuru Mheshimiwa Rais, kwa hatua yake thabiti kwa maslahi ya Uganda.”, aliandika Spika Anita Among.
Mshukiwa aliyepatikana na hatia ya “ushoga” anaweza kufungwa jela hadi miaka 14, kulingana na sheria.
Toleo la mswada huo uliotiwa saini na Rais Yoweri Museveni haliwafanyi kuwa uhalifu wale wanaojitambulisha kama LGBTQ, jambo linalowatia wasiwasi wanaharakati ambao walishutumu rasimu ya awali ya sheria hiyo kama shambulio baya dhidi ya haki za binadamu.
Lakini sheria mpya bado inataja hukumu ya kifo kwa “ushoga uliokithiri,” ambayo inafafanuliwa kama kesi za uhusiano wa kimapenzi unaohusisha watu walioambukizwa VVU na vile vile watoto na aina zingine za watu walio hatarini.
Ushoga tayari ni haramu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki chini ya sheria ya enzi ya ukoloni ambayo inaharamisha vitendo vya ngono “kinyume na utaratibu wa asili”. Kosa hili linaadhibiwa kwa kifungo cha maisha.
Ikulu ya Uganda katika ukurasa wake wa Twitter imetuma picha ya Museveni kuthibitisha kuwa rais huyo ametia saini muswada.