Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani ameomba radhi kutokana na ukatili uliofanywa na Ujerumani kwa Tanzania, wakati wa uasi wa Majimaji mwanzoni mwa miaka ya 1900 ambapo watu laki 3 waliuawa, na kuwa moja ya maasi ya kupinga ukoloni yaliyomwaga damu nyingi zaidi barani Afrika.
Akiongea kwenye jumba la makumbusho mkoani Songea ulikofanyika ukatili huo, rais huyo amesema, “ningependa kuomba msamaha kwa ambacho wajerumani waliwafanya kwa mababu wa hapa, kilichotokea hapa ni historia yetu ya pamoja, historia ya mababu zenu na historia ya mababu zetu huko Ujerumani.”
Uasi wa Majimaji ulichochewa na sera ya Ujerumani ya kulazimisha wakazi wenyeji kulima pamba kwa ajili ya kuuza nje. Tanzania ilikuwa sehemu ya himaya ya Ujerumani ya Afrika Mashariki ambayo pia ilihusisha Rwanda, Burundi na sehemu za Msumbiji.
Rais Steinmeier alikutana na kizazi cha mmoja wa viongozi wa Maji Maji, Chifu Songea Mbano, ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliouawa mwaka 1906.