Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anaanza ziara ya siku kadhaa nchini Marekani, fursa ya kuwasilisha mpango wake wa amani na kuendelea kuwepo kwa Ukraine katika anga ya kimataifa, zaidi ya miaka miwili na nusu nchi hiyo ikiwa kwenye vita kamili na Urusi.
“Ziara hii itaamua nini kitatokea msimu huu wa vuli.” Akizungumza akiwa katika ndege ya kijeshi iliyompeleka Marekani, Volodymyr Zelensky ametaka kuwahakikishia raia wenzake nchini Ukraine kwamba anapigania nchi yake, anaripoti mwandishi wetu wa Kyiv, Cerise Sudry Le-Du. Atawasilisha kwa mwenzake wa Marekani Joe Biden na washirika wake maelezo ya kina ya mpango wake wa amani, unaoelezwa kuwa “mpango wa ushindi”, unaolenga kukomesha mashambulizi ya Urusi katika nchi yake.
“Tumefika Marekani. Lengo kuu ni kuimarisha Ukraine na kulinda watu wetu wote,” Volodymyr Zelensky amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X. Rais wa Ukraine aliwasili mguu Marekani jioni ya Jumapili, Septemba 22. “Vita hivi vinaweza tu kumalizika kwa amani ya haki kupitia juhudi za kimataifa. Mpango wa ushindi wa Ukraine utakuwa kwenye meza ya washirika wetu wote,” aliongeza.
Rais wa Ukraine atatembelea kwanza kiwanda cha kutengeneza silaha, ambacho sehemu yake ya uzalishaji imetengwa kwa Ukraine. Kisha atasafiri kwenda New York na Washington. Anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lakini pia kukutana na Joe Biden katika Ikulu ya White House kuwasilisha kile anachokiita “mpango wake wa ushindi” kwa Ukraine.