Rais wa Kenya William Ruto amewasili mjini Juba, Sudan Kusini, kwa mazungumzo na Rais Salva Kiir Mayardit kuhusu mchakato wa amani uitwao Tumaini Initiative, ikulu ya Kenya imesema.
Wiki jana, Rais Ruto alifanya mazungumzo na wajumbe wa serikali kutoka Sudan Kusini na pia kukutana na wawakilishi wa vyama vya Upinzani katika Mpango wa amani wa Sudan.
“Makundi hayo mawili yamethibitisha kuwa tayari kusaini makubaliano ya Tumaini, matokeo ya mazungumzo shirikishi,” Ikulu imesema.
Kenya imekuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya Serikali ya Mpito Iliyohusisha Umoja wa Kitaifa na makundi mengine ili kuendeleza Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Mzozo katika Mkataba wa Amani wa Sudan Kusini wa 2018.
Sudan Kusini inajitahidi kujikwamua kutoka kwa athari ya vita vya ndani vilivyoanza nchini humo Desemba 2013 kati ya Rais wa wakati huo Salva kiir na makamu wake Riek Machar.
Zaidi ya raia milioni 4 wamelazimishwa kukimbia makwao. Zaidi ya milioni 2.2 wameondoka nchini kabisa, wakati wengine milioni 2.2 wamehamishwa ndani.