Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona ni vema apange safu ya ushindi ambayo inaweza kufunga magoli zaidi ili kuanzia mwakani Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2025 Uchaguzi Mkuu yakafungwe magoli ya uhakika sio ya kubabaisha.
Akiongea mbele ya Rais Samia wakati wa kuwaapisha Viongozi Wateule Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo Sept 01,2023, Dkt. Mpango amesema.. “Nawapongeza Wateule wote katika nafasi mbalimbali, kama ambavyo Kocha yoyote anafanya Mh. Rais imempendeza amewaamini amebadilisha namba zenu za kucheza mpira, maana Mawaziri karibu wote sura zilezile lakini tumebadilisha nafasi na tukiacha mmoja na Manaibu Mawaziri tukiacha wachache”
“Nawaomba sana, Mh. Rais anataka tija zaidi katika utendaji kwahiyo muende mkashirikiane, mzingatie falsafa ya Mh.Rais ya zile R nne, nami natilia mkazo ile ya kusimamia mabadiliko (Reforms)”
“Mmemsikia Makamu Mwenyekiti (Mzee Kinana), ni muhimu sana muwe na masikio juu ya kero za Wananchi wetu Bara na Visiwani na kuzifanyia kazi, yapo maeneo kelele ni kubwa kila unapokwenda, nikimuangalia Jerry Silaa kwenye ardhi kero kubwa ukaongoze timu yako kuhakikisha kero upande wa ardhi zinashughulikiwa ipasavyo, pia upande wa Maliasili magomvi kati ya Wananchi na Hifadhi zetu ni makubwa Waziri ukashirikiane na mwenzako wa mifugo tunapoteza Watu n.k”
“Mheshimiwa Rais ameona ni vema apange safu ambayo inaweza kufunga magoli zaidi ili twende kuanzia mwakani Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2025 Uchaguzi Mkuu twende tukafunge magoli ya uhakika sio ya kubabaisha”