Baada ya siku 750, Afrika Kusini imetangaza mwisho wa hali ya maafa kitaifa na sasa hakutakuwa tena utaratibu wa kuwazuia watu kutoka nje (lockdown) kwa misingi ya UVIKO-19.
Rais Cyril Ramaphosa alitangaza Jumatatu usiku, akisema hatua zote zilizowekwa wakati wa hali ya maafa ya kitaifa zimetoa matokeo chanya.
Alitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuandaa vituo vya matibabu ili kukabiliana na virusi, kutoa chanjo kwa mamilioni ya watu, kutoa ruzuku ya kijamii ya zaidi ya Sh 50,000 (R350) kwa maelfu ya watu wasio na ajira na kuwezesha mfuko wa misaada ambao ulisaidia biashara wakati wa janga hilo.