Mali zenye kuhusishwa na rapa Sean “Diddy” Combs zilipekuliwa siku ya Jumatatu na maafisa wa serikali.
Idara ya Usalama wa Taifa ilisema ilikuwa imefuata “hatua za kisheria kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea” huko New York, Los Angeles na Miami.
Nyumba mbili zilipekuliwa na polisi huko Los Angeles na Miami kama sehemu ya uchunguzi.
Maafisa hawakutaja sababu za upekuzi huo au ikiwa ulikuwa umefungamana na Bw Combs.
Wawakilishi wa nguli huyo wa hip-hop hawakujibu maombi ya BBC ya kutoa maoni yao siku ya Jumatatu.
Kesi kadhaa za hivi majuzi zimemshutumu Bw Combs kwa utovu wa nidhamu wa kingono.
Mawakili wake hapo awali wamekanusha madai yote yaliyotolewa dhidi yake katika kesi hizo.
Maafisa wa Uchunguzi wa Usalama wa Nchi walifanya upekuzi katika jumba lenye ukubwa wa futi za mraba 17,000 ambapo Bw Combs alitangaza toleo lake la hivi punde la kutoa albamu yake Septemba iliyopita.
Anwani ya nyumba hiyo inahusishwa na kampuni ya kutengeneza filamu ya Mr Combs’ Bad Boy Films.
Maafisa wawili wa kutekeleza sheria waliambia Associated Press kwamba upekuzi huo ulikuwa sehemu ya uchunguzi unaoendelea wa biashara ya ngono.