Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila ametoa wito kwa Viongozi wa Dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuweka misingi Bora ya malezi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuliombea Taifa na Viongozi.
RC Chalamila ametoa wito huo wakati wa Mkutano na Viongozi wa Dini wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo uliokwenda sambamba na Dua na Maombi ya kuliombea Taifa ambapo ameahidi kufanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano na Viongozi hao.
Aidha RC Chalamila ametoa wito kwa Viongozi hao kutumia madhabau zao kukemea matendo maovu ikiwemo Ushoga, Usagaji pamoja na vitendo vya uhalifu katika jamii Ili kudumusha Amani.
Katikati kikao hicho RC Chalamila aliambatana na Watendaji kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali kama DAWASA, TANESCO, TANROAD, TARURA na wataalamu wa Ardhi ambapo amewaelekeza kuwa karibu kushughulikia kero kwenye Taasisi za Dini.
Pamoja na hayo RC Chalamila amewaomba Viongozi wa Dini kujiepusha na Migogoro baina Yao ikiwa ni pamoja na kusemana vibaya jambo linalopelekea mifarakano kwa waumini.
Hata hivyo RC Chalamila amefungua milango kwa Viongozi wa Dini kumshauri kwenye mambo mbalimbali ambapo pia ameahidi kushiriki kwenye mikutano na hafla za kidini atakazoalikwa.
Sanjari na hayo RC Chalamila ametumia Mkutano huo kumshukuru na kumpongeza Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa Kazi kubwa na nzuri anayoifanya kupitia utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Maendeleo.