Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amesema ili vita dhidi ya matumizi ya mkaa iweze kufanikiwa, ipo haja ya kufanya maamuzi magumu katika baadhi ya Mikoa ili kuokoa misitu na vyanzo vya maji ikiwemo maamuzi kupiga marufuku kabisa matumizi ya mkaa.
Amesema Viongozi wana jukumu la kulinda vizazi vijavyo ambapo ameshauri katika siku zijazo, italazimika kwamba nyumba zinazojengwa ni lazima Mmiliki wa nyumba aoneshe miundombinu ya gesi ndani kwake…“Nipo tayari kuendeleza mchakato na Wadau katika kuboresha matumizi ya gesi Dar es salaam, Shule za Serikali kupitia Halmashauri zao ni lazima zitenge bajeti kwa ajili ya mabadiliko haya”
Chalamila amesema hayo ofisi kwake alipokutana na Wafanyakazi wa Taifa Gas Tanzania Limited ambao kupitia ghala lao ambalo lipo Kigamboni na ambalo Ndilo kubwa zaidi nchini wamemuahidi RC kuwa wapo tayari kusambaza gesi katika Mkoa wote wa Dar es Salaam ili kila Mtanzania jijini aweze kupata fursa ya kutumia gesi.
Kupitia Msemaji Angellah Bhoke, wanesema Ipo haja ya wadau kushikana na kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuhakikisha Mkoa wa Dar es Salaam ambao unaongoza katika matumizi ya mkaa , unapunguza matumizi haya “Dar es Salaam inatumia 70% ya mkaa wote unaotumiwa nchini na hii huenda ikaongezeka iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kudhibiti matumizi haya.