Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amepiga marufuku maofisa ardhi kupima viwanja katika eneo lolote kabla Kamati ya Mipango Miji haijaidhinisha.
Aidha, amepiga marufuku upimaji wa viwanja kwenye maeneo yote hatarishi yakiwamo ya pembezoni mwa mito ambayo inaweza kufurika na kusababisha madhara kwa binadamu.
Homera ametangaza marufuku hiyo alipotembelea eneo lililoathirika na maporomoko hayo ambayo yalisababishwa na kumeguka kwa Mlima Kawetere kutokana na mvua ya masika inayoendelea kunyesha jijini humo.
Amesema nyumba zilizoathiriwa na tope hilo zina hatimiliki zilitolewa na jiji hilo na kwamba endapo kamati ya mipangomiji ingekagua eneo hilo kabla ya kuanza kumilikisha watu kuna uwezekano ingezuia madhara hayo.
“Maeneo yote hatarishi ni marufuku kupima viwanja kuanzia sasa, ni lazima kamati ya mipango miji ijiridhishe kwanza kuhusu usalama wa eneo husika ndipo upimaji uendelee,” amesema Homera.
Hata hivyo, viongozi wa mila wameiomba serikali kuwasikiliza wanapotoa maoni yao kuhusu maeneo yanayopimwa kwa ajili ya makazi wakidai kuwa baadhi ya maeneo yana historia ambazo sio za kawaida.
Katibu wa machifu wa Jiji la Mbeya, Michael Ilanga, amesema eneo hilo maporomoko yalianzia miaka ya nyuma paliwahi kuwapo ziwa dogo ambalo baadaye lilipotea na miaka ya karibuni limerejea tena likiwa na umbo dogo.