Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amewataka Viongozi kwenye wilaya zote mkoani humo kukamilisha ujenzi wa Miundombinu ya Madarasa, Mabweni na Matundu ya Vyoo hadi kufikia mwanzo wa muhula mpya wa masomo mwezi januari 2024 ili kuwa tayari kupokea wanafunzi.
Makalla amesema hayo Disemba, 19, 2023 wakati wa Kikao kazi cha Wadau wa Elimu kilichofanyika kwajili ya kuweka Mikakati ya kupokea watoto wanaojiunga na Shule za Awali, Msingi na Sekondari ndani ya Mkoa wa Mwanza hususani ukamilishaji wa Ujenzi wa miundombinu ya Madarasa.
Amesema halmashauri zinapaswa kukamilisha miundombinu ya madarasa ipasavyo kama serikali ilivyoagiza ili kutoa nafasi kwa watoto waliofikia umri wa kujiunga na shule za awali na waliofaulu kwenda sekondari waweze kujiunga mara moja na kwenye hilo Kamati za Usalama na Watendaji lazima washirikiane pamoja na kukomesha utoro kwa wanafunzi.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza Martine Nkwabi amefafanua kuwa jumla ya shule za Msingi 991 za Mkoa huo zilifanya Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi 2023 kwa watahiniwa 92, 655 ambapo watahiniwa 78, 437 ikiwa ni Asilimia 84.7 (Wavulana 36,397 na Wasichana 42,040) wamefaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwezi januari 2024.
Ameongeza kuwa pamoja na uwepo wa miundombinu na vifaa bora shuleni bado watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa wana nafasi ya kuhamasisha wazazi kupeleka watoto shule na kuona namna ya kusaidia kuwepo kwa programu ya chakula shuleni ili kuthibiti utoro shuleni na kwenye suala hilo ameitaja Mwanza kuwa nafasi ya 21 kama Mkoa kutoa Chakula.