Leo Disemba 21, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla ameongoza Kikao Kazi cha Wadau wa Uvuvi na ametoa Siku Saba za kurejesha zana Haramu za Uvuvi na kwamba baada ya hapo Msako Mkali utafanyika na kuwakamata wote wanaojihusisha na Uovu huo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Makalla amesema ifikapo disemba 30 Msako Mkali wa kuwakamata wote wanaojihusisha na Uvuvi Haramu na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kwenye kuthibiti hilo amewataka Maafisa Uvuvi kuwajibika ipasavyo katika kutoa Elimu dhidi ya Madhara ya Uvuvi Haramu ili kukomesha zana na Mbinu haramu kwenye Ukanda wa Ziwa Victoria.
Aidha, amesema uwepo wa Masoko ya bidhaa zisizokubalika ndio chanzo cha uvuvi haramu hivyo jeshi la polisi na mamlaka zingine zizuie suala hilo na ni lazima elimu itolewe mara kwa mara kuelezea madhara ya Uvuvi haramu kwa maendeleo ya ziwa hilo linalotegemewa kwa ukuzaji uchumi.
“Mwaka 2022/23 Serikali imetoa Bilioni 65 kuwezesha wavuvi kwa kuwakopesha boti 158 zenye vifaa vya uvuvi ambapo Mwanza imepata boti 29 pamoja na Mradi wa Vizimba 615 kwa kufugia samaki ambapo Mwanza imepata vizimba 375” Amefafanua Mkuu wa Mkoa.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Hillary Mrosso amebainisha kuwa utafiti kwa njia ya teknolojia ya uwingi unaonesha kuwa wingi wa samaki aina ya Sangara umepungua kutoka tani 621, 254 mwaka 2015 hadi tani 161, 918 mwaka 2022 huku Miaka ya 2018, 2021 na 2022 ikiongoza.
“Uwingi wa dagaa umeonekana kupungua kutoka tani 859, 931 mwaka 2015 hadi 321, 392 mwaka 2017 na kwamba uwingi wa Uduvi umekua ukiongezeka katika vipindi mbalimbali.” Amefafanua Mtafiti Mwandamizi Mrosso.
Akitoa wasilisho la Sekta ya Uvuvi, Afisa Uvuvi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Titus Kilo amesema uzalishaji wa Mazao ya Samaki kwenye Viwanda Mkoani Mwanza umepungua kwa asilimia 30 kwa siku kutoka tani 455 hadi 319 na hali hiyo imepelekea kupungua kwa siku kufanya kazi hadi siku 3 kwa wiki huku wafanyakazi wakipungua kutoka 3600 hadi 1800.
“Usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje ya nchi umepungua kutoka tani 8, 356 kwa mwaka 2021/22 hadi tani 7, 112 mwaka 2022/23 ambapo ni sawa na asilimia 14.” Amebainisha Mtaalam huyo wa Kilimo wakati akiwasilisha mada.
Katika kukabiliana na upungufu mkubwa wa mazao ya samaki Kilo ameshauri serikali kuboresha kanuni zinazotaja nyavu zinazofaa kuvulia dagaa kwa kuweka vipimo halisi na kujenga mizani kwenye vituo vyote vya kukusanyia mazao ya Uvuvi pamoja na kuwa na kanzidata ya wavuvi na kubainisha wanaojihusisha za uvuvi haramu na kuwafungia.