Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Solomon Mndeme ameshiriki katika Tamasha la Sanjo ya Busiya ambalo limefanyika katika Kijiji cha Negezi Kata ya Ukenyenge Wilaya ya Kishapu hapa Mkoani Shinyanga na kuwapongeza sana waandaaji kwakuwa tamasha hili limeanza rasmi tarehe 1 Julai, 2023 na linatajwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 10,000 kutoka pande mbalimbali na kwamba huu ni mwaka wa 13 tangu kuanzishwa kwa tamasha.
Pamoja na pongezi nyingi kwa ma Chifu na uongozi wote kwa kufanikisha sherehe hizi lakini pia amewasihi kukemea kwa nguvu zote mmomonyoko wa maadili ambao unaweza kuharibu jamii yetu na vizazi vyetu kwa ujumla huku akiwakumbusha watambue kazi njema anayoifanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, miundombinu, ustawi wa jamii huku akiwataka kumuunga mkono kwa kazi zote za kuwaletea maendeleo wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme.
“Ndugu zangu wanaTamasha la Busiya nawapongeza sana kwa kufanikisha vyema tamasha hili muhimu ambalo limehudhuriwa na watu zaidi ya elfu kumi kutoka ndani na n nje ya Mkoa wa Shinyanga, lakini pia niwakumbushe ndugu zangu kuendelea kusimamia maadili yetu ya Kitanzania na tuendelee kumuunga mkono Rais wetu kwa kazi kubwa na njema ambazo anazifanya katika kutuletea maendeleo sisi wananchi,” amesema Mhe. Mndeme.
Serikali imepokea changamoto zote zilizowasilishwa na Chifu Edward na kwamba zitashughulikiwa kulingana na zilivyo kwakuwa zipo za kisera na kibajeti.
Kwa upande wake Mtemi wa Busiya Ndugu Edward Makwaiya aliipongeza sana Serikali kwa kazi inazozifanya kwa wananchi huku akiomba Serikali kuanzisha Chombo Maalumu kiwe na Mamlaka kama zilivyo Mamlaka nyingine ili waweze kuwa na maamuzi katika kuisaidia Serikali kupambana na mila potofu zenye kuharibu jamii.
Mtemi wa Busiya Ndugu Edward Makwaiya.
Aidha Mtemi Mwakwaiya amesema kuwa lengo la tamasha hilo ni pamoja na kumshukuru Mungu kwa mwaka uliopita, na kukaribisha mwaka mwingine ikiwa ni pamoja na kudumisha tamaduni na kuwaelimisha wananchi wote kuacha kuiga utamaduni wa nje na kuhamasisha utalii wa ndani kwa mashindano ya ngoma za jadi.