Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, ameagiza kuchukuliwa hatua kwa Wakuu wa Idara ambao watazalisha hoja mpya za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama hatua ya kuimarisha utendaji kazi kwenye Halmashauri hizo.
Dendego ametoa kauli hiyo katika Kikao Maalum cha kujadili hoja za CAG cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida ambapo amesema Halmashauri hiyo imekuwa na hoja 64 kutoka mwaka wa fedha 2011 hadi Juni 2024 ambazo hazijafungwa jambo ambalo linatia dosari utekelezaji wa sheria,kanuni na taratibu za Serikali hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Sataki kusikia uzalishaji wa hoja mpya zinazalishwa na kama zikitokea basi aliyesababisha hoja hizo aitwe na kuhojiwa kwa nini hoja hiyo imetokea ikiwezekana achukuliwe hatua kwa kusababisha hoja hiyo hoja hizo zinapotokea zinasababishwa na kuwepo kwa kasoro hasa katika usimamizi hafifu wa miradi ya maendeleo” Halima Dendego RC Singida
Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga ameonyesha kukerwa na uwajibikaji hafifu wa Watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida katika kujibu hoja za CAG licha ya ushauri unaotolewa kwenye kikao cha Kamati ya Fedha.