Jitihada zilizofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) za kufukua Mto Mambi zimerejesha furaha kwa wakazi wa Kijiji cha Chamoto na Uhambule ambapo wameondokana na athari ya nyumba zao kusombwa na maji na mazao yao kuathiriwa.
Afisa Mtendaji Kijiji cha Chamoto Bi. Sekelaga Mwakapesa amesema urejeshaji wa kingo za maji kwa kufukua Mto huo umesaidia sana wakazi wa Kijiji chake kwa kuondokana na adha ya makazi na mazao yao kusombwa na maji hali iyowarudisha nyuma kimaendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Uhambule Bw. Robert Kinanda ametoa shukrani kwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapelekea mradi wa RGROW ambao ndio umefanikisha kutoa Fedha za kufukua Mto Mambi ambao ulikuwa umepoteza uelekeo wake wa asili kutokana shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi na kuwasaidia kumaliza kilio cha muda mrefu kilichokuwa kinahatarisha maisha yao.
Aidha Mwenyekiti wa watumiaji maji Bonde la Mto Mambi anayesimamia kata nne wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya, Bw. Japhet Mtafya amesema wamefanikisha kuondoa adha hiyo baada ya mradi wa REGROW kuchimba kilomita 15 pamoja na kuongeza kina cha mto huo kwa gharama ya shilingi Milioni 200 kwa kutumia wataalamu wa ndani chini ya Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji na kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni Moja kama wangetumia wakandarasi wengine.
Katika kuhakikisha vyanzo vya maji wilaya ya Mbarali vinalindwa na kuwa na tija kwa wakazi wa kata ya Igurusi na maeneo jirani kupia Mradi wa REGROW zimesimikwa ‘beacon’ ili kuonesha mipaka ya kudumu ya vyanzo vya maji, pia shughuli za kibinadamu zisifike katika vyanzo hivyo pamoja na kuweka mabango ya maonyo kwa Wananchi kutovamia maeneo hayo kwa maslai mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.