Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia hali ya hewa, limearifu leo kwamba miezi mitatu iliyopita ilikuwa na joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa duniani.
Shirika hilo limearifu hayo likinukuu takwimu za Idara ya Umoja wa Ulaya inayojijihusisha na masuala ya mabadiliko ya tabianchi la Copernicus Climate Change, na kuongeza kuwa mwezi Agosti ulivunja rekodi ya kuwa na joto kali zaidi kwa tofauti kubwa na wa pili kwa kiwango cha juu cha joto baada ya mwezi Julai, 2023.
Ulaya yakumbwa na matokeo mabaya ya hali ya hewa
Mwezi huo wa Agosti kulingana na shirika hilo ulipindukia wastani wa karibu nyuzi joto 1.5 za Celsius ikilinganishwa na wakati wa kabla ya mapinduzi ya kiviwanda, huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akionya juu ya kitisho dhahiri kitokanacho na mabadiliko ya tabianchi.
Wanasayansi wanalaumu mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu kuwa ya kila mara kutokana na uchomaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi asilia kwa msukumo wa ziada kutoka kwa El Nino ya asili, ambayo ni ongezeko la joto la muda katika maeneo ya Bahari ya Pasifiki ambayo hubadilisha hali ya hewa duniani kote.
Kwa kawaida El Nino, ambayo ilianza mapema mwaka huu, huongeza joto la ziada kwa viwango vya joto duniani lakini zaidi katika mwaka wake wa pili.