Ripoti inaeleza kuwa, vifo vingi vilivyosababishwa na matukio ya ugaidi vilisajiliwa mwaka jana katika eneo la Sahel barani Afrika ikilinganishwa na huko kusini mwa Asia katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.
Ripoti mpya ya Fahirisi ya Ugaidi Duniani 2023 inaeleza kuwa idadi ya wahanga wa mashambulizi ya kigaidi katika eneo la Sahel Afrika imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 2,000 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.
Burkina Faso ni nchi ya kwanza barani Afrika na ya pili iliyoathirika pakubwa duniani haya yamebainishwa kwa mujibu wa Fahirisi ya Kimataifa Kuhusu Ugaidi mwaka 2023 (GTI) kupitia ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Uchumi na Amani (IEP).
Eneo la Sahel lililo chini kidogo ya jangwa la Sahara sasa ni kitovu cha ugaidi.
Ripoti ya Taasisi ya Uchumi na Amani (IEP) imeongeza kuwa, watu 22,074 waliuawa katika mashambulizi 6,408 ya kigaidi kati ya 2007 na 2022 katika eneo la Sahel.
Kwa kuwa na wahanga 8,564 wa ugaidi, Burkina Faso imetajwa kushika nafasi ya pili duniani kutokana na kuathiriwa zaidi na hujuma za kigaidi mwaka uliopita wa 2022 ikiwa nyuma kidogo ya Afghanistan.
Somalia, Mali na Syria zinashika nafasi ya 3,4 na 5 kwa utaratibu. Nchi zinazofuata kwa kuathiriwa pakubwa na hujuma na mashambulizi ya kigaidi baada ya hizi ni Pakistan, Iraq, Nigeria, Burma na Niger.