Leo May 15, 2017 Rais Magufuli ameivunja rasmi Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kuagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Rais ameivunja CDA kwa kutia saini hati ya Amri ya Rais ya kuivunja Mamlaka hiyo Ikulu Dar es Salaam, tukio ambalo limeshuhudiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa, Waziri wa Ardhi William Lukuvi.
Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Antony Mavunde, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana na viongozi mbalimbali wa wizara.
Rais Magufuli amesema ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mgongano wa utoaji wa huduma uliokuwa ukisababishwa na vyombo hivyo viwili na pia kuendana na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa CDA.
Kufuatia uamuzi huo Magufuli pia ameivunja Bodi ya CDA, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CDA Eng. Paskasi Muragili atapangiwa kazi nyingine na ameagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kadiri inavyofaa.
VIDEO: Katika hili lazima nimshukuru Rais Magufuli’ – Maftaha Nachuma. Tazama hapa chini