Utambulisho wake kama binadamu maarufu zaidi kuwahi kuishi duniani hauna mjadala, Cristiano Ronaldo amepata zaidi ya wafuasi milioni 3.5 katika akaunti yake mpya ya YouTube ndani ya masaa matatu (03) baada ya kuifungua.
Ameweka rekodi ya kuwa binadamu wa kwanza kuwahi kufikia wafuasi milioni 3.5 kwenye YouTube ndani ya muda mchache zaidi akiwa na wastani wa wafuasi wapya milioni moja ndani ya dakika tisini (90) za kwanza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 39 na mshindi mara tano wa Ballon d’Or anachezea klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia na ameiwakilisha Ureno katika michuano ya kimataifa kwa zaidi ya miongo miwili.
“Kusubiri kumekwisha. Kituo changu cha @YouTube hatimaye kimefika! Subscribe na ujiunge nami katika safari hii mpya,” Ronaldo alichapisha Jumatano hii ujumbe huo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Saa chache baada ya kuchapisha video yake ya kwanza katika mtandao huo, watumiaji milioni 1.69 walikuwa wamejiunga na chaneli yake mpya, mchezaji huyo ametunukiwa tuzo maalum ya rangi ya dhahabu kutoka You Tube kwa kufikisha idadi ya wafuasi zaidi ya milioni moja.
Mtandao wa You Tube una utaratibu wa kutoa tuzo kwa watumiaji wake, wanapofikisha idadi ya juu ya watu wanaowafuatilia akaunti zao, tuzo ya rangi ya Dhahabu: Unapofikisha wateja 1,000,000. Almasi: Unapofikisha wateja 10,000,000. na Almasi Nyekundu: Unapofikisha wateja 100,000,000.
Ronaldo ana wafuasi milioni 112.5 kwenye jukwaa la X, milioni 170 kwenye Facebook na milioni 636 kwenye Instagram, mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid na Manchester United anajiandaa kwa mechi ya ufunguzi ya Ligi ya Saudia, kati ya timu yake dhidi ya Al-Raed leo Alhamisi, Agosti 22, 2024.