Kikosi maalum cha Sudan (RSF) kimelaani mauaji ya gavana wa jimbo la Darfur Magharibi, Khamis Abbakar, siku ya Jumatano.
Gavana wa jimbo la Darfur Magharibi Khamis Abakar aliuawa baada ya mahojiano ya televisheni akiwashutumu wapiganaji wa kijeshi kwa kuua raia kwa wingi na kutoa wito wa kuingilia kati kimataifa.
Kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari mbalimbali hapo awali, maafisa wa Sudan walishutumu RSF kwa kumuua gavana huyo – ambaye masaa machache kabla ya hapo alisema RSF na wanamgambo washirika walikuwa wakifanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa jamii ya Masalit.
Lakini katika taarifa, RSF inasema gavana huyo aliuawa “mikononi mwa wahalifu wawili” licha ya majaribio ya vikosi vyake kumlinda.
Wiki hii zaidi ya wanafunzi 13,000 kutoka mji mkuu wa Sudan Khartoum walifanya mitihani yao ya mwisho wa mwaka wa shule ya sekondari umbali wa mamia ya kilomita, huko Port Sudan.
Jiji limesalia kuwa tulivu tangu mapigano yalipozuka katikati ya mwezi wa Aprili kati ya jeshi na kundi la wanamgambo wa RSF.
Mapigano hayo yaliendelea bila kusitishwa siku ya Jumatano katika sehemu za mji mkuu, Khartoum, na eneo la magharibi la Darfur – maeneo ambayo yameshuhudia mapigano mabaya zaidi hadi sasa huku takriban raia 959 wakiuawa na wengine wapatao 4,750 walijeruhiwa kufikia Juni 12, kulingana na Shirika la Madaktari la Sudan, linalofuatilia vifo vya raia.
Kundi hilo la matibabu lilisema idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi ikizingatiwa kwamba haikuweza kuzingatia wale waliouawa au kujeruhiwa katika mapigano yanayoendelea huko el-Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi.
Hospitali za jiji hilo zimekuwa hazifanyi kazi tangu mapigano yalipozuka huko mwezi wa Aprili, kundi hilo lilisema.