Mfanyabiashara James Rugemalira ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi yake hautokamilika hadi Upande wa Mashtaka ufuatilie barua aliyomuandikia Kamishina Generali wa (TRA).
Rugemalira ameandika barua hiyo kwa Kamishina wa TRA akielezea ni jinsi gani benki ya Standard Charter Hong kong walivyokuwa wakikwepa kodi na ushuru wa forodha.
Hayo yameibuka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa TAKUKURU, Maghela Ndimbo kudai kuwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka 2017 imeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.
Baada ya kueleza hayo, Rugemalira alidai kuwa Januari 24, 2020 aliongea na mwakilishi wa TAKUKURU alipotembelea gerezani na akamkabidhi nakala ya barua hiyo aliyoandika kwenda kwa Kamishna wa TRA lakini hadi sasa hajapata jibu lolote.
“Naomba kesi ikitajwa upande wa Mashitaka walete jibu kwa sababu wanaostahili kushitakiwa katika kesi hii ni benki hiyo na ninashangaa kuona wengine wanaongezwa katika kesi kwa madai upelelezi haujakamilika,” Rugemalira.
Pia alidai upelelezi wa kesi hiyo hautakamilika na ili ukamilike wafuatilie hiyo barua aliyowapelekea.
Baada ya Rugemalira kueleza hayo, Hakimu Shaidi aliiahirisha kesi hiyo mpaka Februari 13, 2020 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Mbali na Rugemalira, wenzake ni Harbinder Sethi ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL) na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni hiyo, Joseph Makandege.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2017, Makandege anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 980,000 pia yapo ya utakatishaji wa Fedha.
Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka hayo Desemba 20,2019,baada ya kuunganishwa na washtakiwa Seth na Rugemalira katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi.
Miongoni mwa mashtaka hayo ,Makandege anadaiwa kuwa, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, akiwa na wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Pia anadaiwa kuongoza genge la uhalifu, katika nchi hizo, akiwa si mtumishi wa Serikali akishirikiana na watumishi wa umma kwa kuratibu na kufadhili mpango wa uhalifu.
Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Makandege anadaiwa kuwa kati ya Januari 23, 2014 na Februari 2014, alijipatia dola 380,000 katika benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni na dola 600,000 katika benki ya UBL Bank(T) Ltd iliyopo wilaya ya Ilala, fedha zilizotoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa nyakati tofauti.
Kwa upande wa washtakiwa Sethi na Rugemalira walifikishwa mahakamani hapo zaidi ya miaka miwili wamekaa rumande, kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokukamilika.
Washitakiwa Seth na Rugemalira kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017.
Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.
Aidha, inadaiwa katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27.
Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.