Rais William Ruto amepongeza idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukubali vikosi vya kigeni kuhudumu nchini Haiti ili kudhibiti ghasia za magenge ya kihalifu ambayo yametikisa mji mkuu wa nchi hiyo Port-au-Prince kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne, Rais Ruto alikaribisha uamuzi wa baraza hilo, akiutaja kuwa ” chombo muhimu cha kufafanua juhudi za kimataifa kudumisha usalama nchini Haiti.
“Hali ya Haiti inadai, kama suala la kuzingatia kibinadamu, uwajibikaji wa kimaadili na haki ya kimsingi, kwamba hatua zinapaswa kuongezwa kwa kiasi kikubwa ili kukidhi mahitaji ya misaada ya dharura, misaada ya kibinadamu, afya ya umma na ulinzi,” Rais Ruto alisema.
Baraza hilo lenye wanachama 15 mnamo Jumatatu lilipitisha azimio linaloidhinisha ‘oparesheni ya Usalama wa Kimataifa chini ya uongozi wa Kenya kusaidia polisi wa Haiti katika kupambana na magenge hayo.
Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani na Ecuador, liliidhinishwa kwa kura 13 huku China na Urusi zikijizuia kupiga kura.