Mapema hii leo Tarehe 11 Julai 2024, Rais William Ruto ametangaza kulivunja Baraza lake la Mawaziri na kuwaondoa makatibu wote katika Baraza la Mawaziri akiwemo Mwanasheria Mkuu. Mnamo Julai 5, Ruto alitangaza hatua kadhaa za kupunguza gharama za matumizi katika mashirika mbalimbali ya serikali.
Ruto amefanya maamuzi ya kubaki na naibu wa Rais na Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Yote yanajiri baada ya muswada wa fedha ulioleta taharuki na maandamano nchini humo kufutiliwa mbali na Rais Ruto, ambapo maandamano hayo yalisababisha vifo vya takriban watu 41.
Akilihotubia taifa la Kenya hii leo katika Ikulu ya Taifa Ruto alisema, “Leo, kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Ibara ya 1521 na 1525 B ya katiba na kifungu cha 12 cha sheria ya mwanasheria mkuu, nimeamua kuwafuta kazi mara moja katibu wa baraza la mawaziri na mwanasheria mkuu wa Jamhuri ya Kenya.”
Wiki iliyopita, Ruto alipendekeza kupunguzwa kwa matumizi ya serikali na kukopa hela nyingi zaidi ili kujaza pengo la bajeti la takriban dola bilioni 2.7.
Pengo hili lilisababishwa na uamuzi wa kufuta nyongeza ya kodi iliyopangwa kufuatia maandamano ya nchi nzima pia Ruto akitaja mabadiliko yajayo kwa serikali. Muswada wa fedha ambao haukutiliwa saini na Rais Ruto, ulileta hali ya ukakasi kwa wananchi wengi nchini Kenya hususani vijana ambao wanajulikana kwa jina la ‘Gen Z’ ikileta maandamano makubwa zaidi nchini humo ambapo hivi karibuni hadi Bunge lilivamiwa na wananchi.