Muda wa Ruud van Nistelrooy na Manchester United umefikia kikomo, klabu hiyo imethibitisha siku moja baada ya Mholanzi huyo kuiongoza timu hiyo kushinda mabao 3-0 dhidi ya Leicester City kwenye Ligi Kuu ya Uingereza katika mchezo wake wa nne kama meneja wa muda.
Kuondoka kwa Van Nistelrooy kulitangazwa Jumatatu huku Ruben Amorim akiwasili Manchester kama bosi wa kudumu wa United.
“Ruud ni, na daima atakuwa, gwiji wa Manchester United,” klabu hiyo ilisema katika taarifa.
“Tunashukuru kwa mchango wake na jinsi ambavyo ameshughulikia jukumu lake katika kipindi chote alichokuwa na klabu. Daima atakaribishwa sana Old Trafford.”
Wasaidizi wa United Rene Hake, Jelle ten Rouwelaar na Pieter Morel pia waliondoka siku ya Jumatatu, huku klabu hiyo ya Old Trafford ikisema watatangaza wafanyakazi wa Amorim baadaye.