Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania Dkt. Said Mohamed amesema kati ya ruzuku ya mitihani iliyokuwa imepangwa 83% imeshatolewa mpaka kufikia Mwezi Februari 2024 ambapo imewezesha kutekeleza malengo ya Taasisi.
Akizungumza Machi 15, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipotembelea Baraza hilo kujionea namna fedha zilizotengwa katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24 zilivyotumika.
Dkt. Mohammed amesema kuwa fedha hizo zimetumika katika uchakataji na utoaji wa matokeo ya Mitihani ya kidato cha Sita na Ualimu 2023, kuendesha Mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la nne, Kidato cha pili na mitihani mingine iliyofanyika 2023 na 2024.
Ameongeza kuwa kazi zizonaendelea kutekelezwa ni pamoja na uchapaji wa vyeti vya watahiniwa wa Mtihani wa Kidato cha Nne 2023, kuchapa vyeti vya watahiniwa wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi 2023, kuendesha Mitihani ya Kidato cha Sita na Ualimu 2024 na vyote viko katika hatua nzuri.