Timu ya Taifa ya Riadha inayoshiriki mashindano ya Dunia ya Riadha yanayoendelea London itaanza kibarua cha kuipeperusha bendera ya Tanzania August 5, 2017 ambapo Mwanariadha Failuna Abdi Matanga atakimbia mbio za mita 10,000 ambapo atakuwa na nafasi kubwa ya kushangiliwa na Watanzania moja kwa moja kupitia DStv kuanzia Saa mbili Usiku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema DStv imefanya jitihada kubwa na kuhakikisha watanzania wanaishuhudia timu yao ikiwawakilisha katika mashindano hayo muhimu ulimwenguni.
>>>“Tunawahakikishia watanzania burudani hii moja kwa moja kupitia DStv chaneli za Supersport. Tunaamini sote tutakuwa nyuma yao wachezaji wetu kuwashuhudia jinsi wanavyotuwakilisha.” – Maharage Chande.
Mbali na Failuna Watanzania pia watawashuhudia Alphonce Felix Simbu, Ezekiel Jafari Ng’imba na Stefano Huche Gwandu ambao watakimbia mbio ndefu za Kilomita 42 siku ya Jumapili kuanzia saa nne Asubuhi.
Wanariadha wengine watakaotazamwa na Watanzania kupitia DStv Jumapili August 6, 2017 ni wanawake Sara Ramadhani Makera na Magdalena Crispin Shauri ambao watakimbia Kilomita 42 majira ya saa nane mchana huku Wanariadha wengine wawili wa mbio fupi za mita 5,000 ambao ni Emmanuel Giniki Gisamoda na Gabriel Gerald Geay wao watakimbia Jumatano August 9, 2017 saa mbili usiku ikiwa ni raundi ya mchujo na endapo watafuzu watashiriki fainali ya mita 5,000 Jumamosi August 12, 2017 ambapo pia watashuhudiwa LIVE kupitia DStv.