Viongozi wa Jumuiya ya maedeleo ya Kusini mwa Afrika, (SADC) wamekubali kupeleka wanajeshi kusaidia kudhibiti uasi unaofanywa na kikundi cha wanamgambo wa Kiislam kinachofanya mauaji na kusababisha taharuki kaskazini mwa Msumbiji kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.
“SADC imeidhinisha kupelekwa kikosi cha dharura kuisaidia Msumbiji kupambana na ugaidi na vitendo vya uhalifu unaotokana na misimamo mikali huko Cabo Delgado,” Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Stergomena Tax amesema mwishoni wa mkutano wao wa siku moja. Hakufafanua ukubwa wa kikosi hicho na muda wa kwasili nchini Msumbiji.
Akihutubia katika mkutano Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema “Tunatambua na kuridhia mshikamano na msaada wa nchi wanachama wa SADC na nchi rafiki ambao wanaunga juhudi kuzuia ugaidi kupata sehemu mwaafaka kuendesha mashambulizi katika nchi zetu na kanda zima.”
Waraka uliopatikana kwa siri mapema mwaka 2021 ulikuwa unapendekeza kupelekwa takriban wanajeshi 3,000 katika mkoa wa Cabo Delgado, ambapo waasi wameviteka vijiji na miji kadhaa, na kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
Ghasia zimeongezeka katika sehemu za kaskazini mwa Msumbiji lenye utajiri wa gesi uliopatikana mwishoni mwa 2017 na kuna wasiwasi zinaweza kuenea katika nchi jirani.
Hapo Machi 24, wanamgambo wenye uhusiano na kikundi cha Islamic State walianzisha mashambulizi mbalimbali yaliyopangwa kufanyika wakati mmoja katika mji wa kaskazini wa Palma, ikiharibu majengo na kuua wakazi huku maelfu yao wakikimbilia msituni.