Mashirika ya ndege yamefuta leo mamia ya safari zake za kuingia na kutoka viwanja vya ndege vya Ujerumani baada ya wafanyakazi wa usalama kufanya mgomo wa kudai nyongeza ya mishahara.
Wahudumu wa usalama walisusia kazi katika viwanja sita vya ndege vikiwemo vya Düsseldorf, Cologne/Bonn na Berlin, na migomo ya siku moja pia imeitishwa katika viwanja vingine vya ndege kesho Jumanne vikiwemo vya Frankfurt na Hamburg.
Mgomo huo unafanyika wakati mashirika ya ndege yakiyumba kutokana na athari za vita vya nchini Ukraine, huku kukiwa na ongezeko la bei za mafuta na kufungwa kwa anga, baada ya miaka miwili ya mahitaji ya chini ya safari kutokana na janga la virusi vya corona.