Bunge la Congress lilipitisha muswada huo kutokana na wasiwasi juu ya usalama wa taifa na ni kwasababu ya uhusiano wa TikTok na taifa la China.
Wabunge na wataalam wa usalama walisema kuna hatari kubwa ya serikali ya China kuegemea na kushinikiza kampuni ya ByteDance kuwapa taarifa nyeti za watumiaji milioni 170 kutokea nchini Marekani au kueneza propaganda.
Sheria hii mpya itaruhusu TikTok kuendelea kufanya kazi nchini Marekani ikiwa ByteDance itaiuza ndani ya siku 270 au takriban miezi tisa, muda ambao rais anaweza kuongeza kufikia mwaka 1.
Hatua hii huenda ikakabiliwa na changamoto za kisheria, pamoja na upinzani unaowezekana kutoka kwa Serikali ya China, ambao unaweza kuzuia uuzaji au usafirishaji wa teknolojia hiyo. Mpaka sasa haijulikani pia ni nani aliye na rasilimali ya kununua TikTok, kwani itakuwa dau kubwa sana.
Uuzaji wa jukwaa la Tiktok unaweza kuchukua miezi au hata miaka kusuluhishwa, wakati ambapo programu ingeendelea kufanya kazi kwa watumiaji wa nchini Marekani.
Kampuni ya TikTok imeahidi kupinga sheria hii mpya dhidi yao ambapo kupitia jukwaa lao CEO ama afisa mtendaji wao Shou Chew alifunguka kwa njia ya video akisema Wanajiamini ya kwamba wao hawaendi popote na kwamba wataendelea kupigania haki zao na haki za watumiaji mahakamani.
Akiendelea kwa kusema taarifa zote za wamarekani wapatao Milioni 170 zilizohifadhiwa na Tiktok zipo salama na wanaendelea kutumia njia nyingi ilikuboresha usalama wa taarifa hizi huku wakipambana kuendelea kulisimamia jukwaa lenye biashara Milioni 5 za Wamarekani wanaotegemea application hiyo kujipatia kipato.