Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amekataa kutia saini muswada mpya unaoeleza hukumu ya kifo katika baadhi ya kesi dhidi ya ushoga ambapo ameomba muswada huo ufanyiwe marekebisho kwa kuongezewa ukali zaidi kabla ya yeye kutia saini na kuifanya kuwa sheria.
Museveni pamoja na mambo mengine ametaka pia sheria irekebishwe ili kuwaruhusu Watu wanaokataa kwa hiari yao vitendo vya ushoga wapitie hatua za urekebishaji au waweze kupatiwa matibabu ya kuwabadilisha na kuwaweka sawa licha ya kwamba hatua hizo zimekataliwa na Mashirika ya matibabu kuwa hazifai na zinaweza kuleta madhara ya afya ya akili kwa wanaobadilishwa tabia.
Uamuzi huo wa Museveni umetangazwa baada ya mkutano wa Wabunge ambao takribani wote wanaunga mkono muswada ulioidhinishwa na Wabunge mwezi uliopita, Museveni amepewa siku 30 za kusaini muswada huo ili iwe sheria na kuirejesha Bungeni ili ifanyiwe marekebisho na kumjulisha Spika wa bunge kwenye maamuzi, hata hivyo, inaweza kupitishwa kuwa sheria bila kibali cha Rais iwapo muswada huo utarudishwa Bungeni mara mbili.
Muswada huo katika hali yake ya sasa umependekeza adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kufanya mapenzi ya jinsia moja hadi miaka 14 kwa kosa la ushoga na kifungo cha miaka 20 jela kwa kuajiri, kukuza na kufadhili shughuli za mapenzi ya jinsia moja.