Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah atapatikana tu kwenye fainali ya Kombe la Ligi ya England dhidi ya Chelsea dakika za mwisho, meneja msaidizi Pep Lijnders alisema Ijumaa.
Wachezaji wengine wawili tegemeo, mshambuliaji Darwin Nunez na kiungo Dominik Szoboszlai, wako katika hali sawa kutokana na majeraha waliyoyapata kabla ya mchezo wa Jumapili utakaopigwa kwenye Uwanja wa Wembley.
“Bado tuna siku mbili – kwa hivyo kikao cha leo na cha kesho – na dakika ya mwisho tutaangalia kama wanaweza kuwa huko,” Lijnders aliambia mkutano na waandishi wa habari.
Salah alipata uchovu wa misuli na hakucheza katika ushindi wa katikati ya wiki wa Liverpool dhidi ya Luton. Aliumia msuli wa paja wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa na Misri.
Nunez pia alikosa mchezo wa Jumatano baada ya kubadilishwa wakati wa mapumziko katika ushindi wa 4-1 wa Liverpool dhidi ya Brentford Jumamosi iliyopita. Szoboszlai ana tatizo la misuli ya paja.