Leo December 22. 2017 Serikali ya Tanzania na Uganda zimesaini makubaliano mengine ya kuboresha sekta ya mifugo ili kuimarisha ushirikiano wa kuthibiti magonjwa hatari ya mlipuko na kuanzisha minada ya pamoja ya kimataifa kwa maslahi ya nchi zote mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa ikiwa tayari kuna makubaliano yaliyosainiwa na nchi hizi mbili kuhusu bomba la mafuta kutokea Uganda hadi mkoani Tanga, Tanzania.
Makubaliano yamefanyika leo mjini Bukoba ambapo upande wa Uganda uliwakilishwa na Balozi wake nchini, Richard Tumusiime Kabonero na kwa Tanzania akiwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo Dk. Mary Mashingo.
Akizungumza mara baada ya utiaji wa saini makubaliano hayo Balozi Kabonero amesema magonjwa ya mlipuko kwa wanyama hayana mipaka hivyo makubaliano yaliyofanyika yatasaidia kudhibiti magonjwa ya wanyama hatimaye kuboresha mifugo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo Dr. Mashingo amesisitiza kwamba ushirikiano wa kitaalam katika kuratibu, kufuatilia hali ya mifugo na kufanya tathmini ya kila wakati utaleta mafanikio makubwa baina ya nchi ya Tanzania na Uganda.
“Ili kuboresha masoko ya mifugo baina ya Uganda na Tanzania tumekubaliana kuwa na minada ya kimataifa katika maeneo ya Mtukula kwa upande wa Tanzania na Kamwema kwa upande wa Uganda,”– Dr. Mashingo