Leo August 30 2018 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania Agnes Kijo amewataka watoa huduma ya vyakula kwenye mikusanyiko ikiwemo kwenye Misiba na Harusini wajisajili.
Akizungumza na waandishi wa habari Kijo amesema utoaji wa huduma ya chakula unapaswa kuzingatia Sheria na Kanuni Bora za Usafi ili kuhakikisha chakula kinachoandaliwa ni salama.
“Mitindo ya maisha imebadilika kumekuwa na ongezeko la uhitaji wa chakula katika mikusanyiko kama vile misiba, mikutano,maofisini na harusini jambo ambalo linapaswa kuzingatia sheria,”amesema.
Kijo amesema kuwa kwa sasa TFDA itakuwa na kazi ya kutoa elimu kwa watoa huduma hao ambapo watatoa muda maalum ili watu wajisajili baada ya hapo wataanza ukaguzi kwa kila halmashauri.
Pia amesema kuwa itafikia hatua wataanza kusimamisha magari yaliyobeba vyakula ili kuyakagua.
“Hatutotaka tufikie hatua ya kufungiana biashara, kufikishana mahakamani bali tunahitaji watu wafate sheria kwa kujisajili ili watambulike na huduma wanazozitoa zizingatie usafi,“amesema.
Kijo amesema kuwa imeshuhudiwa watu wakiugua na kupoteza maisha ambapo hali hiyo inatoa picha juu ya umuhimu wa kutoa kipaumbele katika masuala ya usalama wa chakula.