Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewaagiza Makamanda wa Polisi nchini washirikiane na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuchunguza na kuwakamata wapinzani wanaomtukana Rais pamoja na Serikali kwa ujumla kupitia vikao vyao vya ndani vya siasa.
Akizungumza Mjini Kilosa katika mkutano wa hadhara Lugola amesema ana taarifa kuna baadhi ya wapinzani ambao wanafanya vikao vyao vya ndani huku wakitukana, kubeza pamoja na kuwachonganisha wananchi na Serikali yao ambayo inaongozwa na Rais Dkt John Magufuli.
Kutokana na wapinzani hao kuvunja agizo lililowekwa, amewaagiza Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya nchini kuwachunguza viongozi wa vyama vya siasa kwa kina kupitia vikao vyao, na watakaowabaini wanavunja utaratibu huo wawakamate haraka iwezekanavyo.
“Mimi Waziri sitakubaliana na kiongozi wa chama chochote kuvunja agizo tulilolitoa nchi nzima kwa kutokuruhusu kufanyika mikutano ya hadhara ya siasa, na pia kupitia mikutano ya ndani ambayo inafanyika, ambapo baadhi ya wanasiasa wahuni wanamtukana Mheshimiwa Rais ambaye ndio kiongozi mkuu wa nchi, mimi sitakubaliana na hilo,” Lugola.
Lugola amewataka wapinzani kuwa wasikivu kwa kufuata sheria za nchi na pia kutambua kuwa, Rais wa nchi hii ambaye kipenzi cha wananchi anapewa heshima yake kwa kuiletea maendeleo nchi.
Lugola amesema Rais Magufuli ni kiongozi ambaye kwa muda mfupi ameiletea mabadiliko makubwa nchi, na pia mipango mikubwa ya maendeleo inakuja katika uongozi wake.
MCHUNGAJI MGOGO KATIKA UBORA WAKE “PASUA KICHWA NI MMEO, UNAWEKA MISUMARI NA BOKO HARAMU”