Jumuiya ya Ecowas inasema sehemu kubwa ya wanachama wake wako tayari kuhusika katika uundwaji wa kikosi maalum kinachoweza kuingilia kati kuhusu kinachoendelea nchini Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi jana.
Wakuu wa majeshi kutoka nchi wanachama 15 wa Ecowas wamekutana jijini Acra nchini Ghana katika kikao cha hivi punde kujaribu kutafuta juhudi za kumrejesha madarakani rais Mohammed Bazoum.
Kwa mujibu wa kamishena wa Ecowas Abdel-Fatau Musah, wanachama wake wote isipokuwa mataifa yanayoongozwa na jeshi na Cape Verde yako tayari kushiriki katika mpango huo.
Jumuiya hiyo kwa muda sasa imekuwa ikiwazia uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi nchini Niger kama hatua ya mwisho iwapo diplomasia haitatua mzozo wa sasa.
Burkina Faso na Mali, ambazo zimekabiliwa na mapinduzi ya kijeshi tangu mwaka wa 2020, zilionya kuwa uiingiliaji wa kijeshi huko Niger utachukuliwa kama kitendo cha kivita.
Kitengo cha usalama katika umoja wa mataifa kilikutana siku ya Jumatatu kuwazia kuhusu suala la matumizi ya kijeshi jijini Niamey japokuwa uamuzi wake haujaekwa tayari.