Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Sekta ya elimu ni wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika kuleta maendeleo ya nchi.
Amesema kuwa utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo. “Ili kufanikisha haya tunahitaji sekta hii kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa”.
Amesema hayo leo (Jumatatu, Machi 25, 2024) wakati wa mkutano wa wadau wa Sekta ya Elimu mkoani Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biblia-TAG jijini Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Suluhu Samia ni mdau namba moja wa sekta ya elimu na ndio maana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake amewekeza katika kuweka mazingira bora ya utoaji elimu na kuhakikisha Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo katika Sekta ya Elimu.
“Ninaamini sisi sote ni mashuhuda wa jinsi Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha uongozi wake alivyotekeleza kwa vitendo azma ya kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa Watoto wote wa Kitanzania bila kujali jinsia wala hali ya kiuchumi”.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa baadhi ya maeneo ambayo Rais Dkt. Samia ameyasimamia kikamilifu ni Mpango wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu, Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi, Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, Mapitio ya Sera Ya Elimu na Mafunzo.
Maeneo Mengine ni Kuimarisha Usimamizi wa Sekta ya Elimu kwa kutoa vyombo vya usafiri kwa viongozi wasimamizi wa elimu pamoja na wathibiti ubora wa shule, Kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji Elimu na kutoa Mafunzo kwa walimu kazini (MEWAKA) kwa ajili ya kuwajengea uwezo na umahiri katika kutimiza majukumu yao.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amewataka viongozi katika halmashauri nchini kuhakikisha fedha zinazoletwa kwa ajili ya kulipa stahiki mbalimbali za walimu zisipangiwe matumizi mengine. “Walimu wapewe stahiki zao mara moja ili kuondoa malimbikizo ya madeni yasiyo ya lazima na manung’uniko dhidi ya Serikali bila sababu”.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Maafisa elimu nchini kuwa na utaratibu wa kwenda vijijini ili kubaino changamoto katika sekta hiyo badala ya kukaa ofisini pekee.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kuwa katika kipindi cha Miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kiasi cha Shilingi bilion 92.4 zimetolewa kwa ajili miundombinu ya elimu mkoani humo.
“Idadi ya shule za msingi za Serikali imeongezeka kutoka 784 mpaka kufikia shule 819 mwaka 2023/2024, wakati shule za Sekondari zimeongezeka kutoka 218 mpaka kufikia 235”.