Selena Gomez amefichua kuwa hawezi kubeba mimba kutokana na matatizo ya kiafya ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yake na ya mtoto.
Katika mahojiano na Vanity Fair, mwigizaji huyo wa Filamu ya “Only Murders in the Building” alisema alitarajia kuanzisha familia ifikapo umri wa miaka 35, lakini changamoto za kiafya zimefanya hilo kuwa gumu.
Gomez, mwenye umri wa miaka 32, hajabainisha tatizo hasa lililopelekea hali hiyo, ingawa amewahi kuzungumzia kuwa na Ugonjwa wa Lupus, ambapo mfumo wa kinga hushambulia tishu na viungo vya mwili, aliwahi kufanyiwa upasuaji wa kupandikizwa Figo mwaka 2017 kutokana na lupus, aidha amepata changamoto za kiakili kama vile wasiwasi, huzuni, na ugonjwa wa Bipolar ambao pia umesababisha haja ya kutumia Dawa zinazoweza kufanya Mimba kuwa hatari.
Ingawa hawezi kubeba Mimba, Gomez alisema yuko wazi kwa njia nyingine za kuwa Mzazi kama vile kuasili au kutumia huduma ya kubeba Mimba kwa niaba.
Anasema anaona ni baraka kuwa, kuna watu wanaosaidia kufanikisha ndoto za kuwa mama kupitia njia hizi.
Kwa sasa, Gomez anasema amekubaliana na hali hiyo na ana matumaini juu ya safari yake ya kuwa Mzazi, hata kama itatofautiana na matarajio yake ya awali.