Watu 16 wamefariki na 22 kujeruhiwa siku ya Jumatatu asubuhi baada ya basi kugongana na lori katikati mwa Senegal, kikosi cha Zimamoto kimesema.
Ajali hiyo imetokea siku ya Jumatatu mwendo wa saa 12:00 asubuhi saa za Senegal kwenye barabara ya kitaifa ya 3, karibu na mji wa Ndangalma, amesema afisa wa zimamoto ambaye ameomba kutotajwa jina.
Ajali za barabarani hutokea mara kwa mara nchini Senegal, ambapo mara nyingi husababishwa na uchakavu wa barabara, magari yanayokiuka viwango vya usalama, kuendesha gari bila kujali, au ufisadi ulioenea miongoni mwa maafisa wa polisi wa barabarani au idara inayohusika na kutoa leseni ya kuendesha gari.
Serikali ya Rais Bassirou Diomaye Faye, aliyechaguliwa mwezi Machi, iliahidi jibu kali katikati ya mwezi Agosti kutokana na ongezeko la ajali za barabarani.
Waziri wa Uchukuzi El Malick Ndiaye ametangaza kuimarishwa kwa ukaguzi wa barabarani na kuimarishwa kwa vikwazo.