Mwalimu wa madrasa nchini Senegal anayeshukiwa kuwabaka wanafunzi wake 27 wa kike alikamatwa Jumatatu baada ya wiki kadhaa za kukimbia chanzo cha polisi kimeliambia shirika la habari la AFP.
Mwalimu huyo anatuhumiwa kuwabaka wanafunzi katika madrasa yake katika mji mtakatifu wa Touba uliopo kati-kati mwa Senegal, afisa wa polisi wa mji huo amesema.
Mshukiwa huyo alitoweka baada ya tuhuma hizo kuibuka mapema mwaka huu kufuatia malalamiko kutoka kwa watu wanaodaiwa kuwa waathirika waliotoa vyeti vya matibabu, chanzo hicho kimeongeza. Alikamatwa siku ya Jumatatu baada ya kujisalimisha kwa polisi. Baada ya kuhojiwa, alikabidhiwa kwa vyombo vya usalama afisa huyo alisema.
Chanzo hicho kimesema mwalimu huyo anatuhumiwa kwa kuwabaka wanafunzi 27, lakini hakutoa maelezo sahihi kuhusu tarehe za madai ya uhalifu au umri wa walalamikaji.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba waliodaiwa kuwa waathiriwa walikuwa “watoto”, ikimaanisha kuwa walikuwa chini ya miaka 15, na kwamba shule ya Kurani imefungwa.
Gazeti la “Le Jour” liliandika wiki iliyopita kuwa kisa hicho kilidhihirika wakati mmoja wa wasichana hao alikataa kurudi shuleni, ambako wanafunzi hujifunza mafundisho ya Kiislamu, kwa sababu mwalimu huyo “alikuwa na mahusiano ya kimapenzi naye na wasichana wengine wote”.