Kinara wa Upinzani nhcini Senegal Ousmane Sonko ameitisha maandamano zaidi kupinga uwezekano wa rais Macky Sall wa kutaka kuwania muhula wa tatu mwaka wa 2024. Imechapishwa: 03/07/2023 – 11:07
Wataalam wa katiba nchini humo wanahisi kuwa iwapo rais Sall atachukua hatua hiyo ya kuwania tena atakuwa amekwenda kinyume na katiba ya taifa hilo.
Wito wa Sonko unakuja wakati huu rais Sall akitarajiwa leo Jumatatu jioni kuweka wazi iwapo atawania muhula watatu madarakani au la kwenye hotuba yake kwa taifa.
Tayari wafuasi wa Chama tawala nchini humo, wameendelea kutetea kile wanachokiita uhalali wa Kiongozi wao kuwania muhula wa tatu ambapo wengi wamesema swala hilo limeshatatuliwa.
Mwezi uliopita, maelfu raia waliandamana katika maeneo tofauti nchini humo baada ya Sonko kupewa kifungo cha miaka miwili jela kwa makossa ya kuwarubuni vijana.
Sonko, wafuasi wake na baadhi ya waangalizi wa mambo wa kisiasa wanasema kuwa hatua hiyo ya mahakama ililenga kumzuia mwanasiasa huyo kuwania katika uchaguzi wa urais ujao.
Makabiliano kati ya wafuasi wa Sonko na maofisa wa polisi yametajwa kuwa mabaya zaidi kutokea nchini humo katika siku za hivi karibuni.
Mwansiasa huyo wa upinzani Jumapili ya wiki iliyopita alisema kuwa iwapo rais wa sasa atatangaza nia yake ya kuwania, raia wote wa Senegali wanafaa kupinga uamuzi wake.
Sall, mwenye umri wa miaka 61 aliingia madarakani mwaka 2012 na kushinda muhula wa pili mwaka 2019. Hata hivyo katiba mpya ya Senegal iliyopitishwa mwaka 2016 inaweka ukomo kwa rais kuongoza kwa mihula miwili ya miaka mitano.
Ingawa Sall hajathibitisha mipango ya kugombea tena, hivi karibuni aliliambia gazeti moja la Ufaransa kwamba anaweza kuwania muhula mwingine kwa sababu muhula wake wa kwanza wa uongozi chini ya katiba mpya ulianza baada ya kuchaguliwa tena mwaka 2019.
chanzo;RFI