Serikali ya Senegal imedumisha marufuku iliyoweka kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok mwezi Agosti.
Mamlaka ilikuwa imepiga marufuku programu hiyo kwa madai kuwa “ilikuwa mtandao unaopendelewa kwa watu waovu kutangaza jumbe za chuki na uasi ambazo zinatishia uthabiti wa nchi”.
Waziri wa Mawasiliano wa Senegal Moussa Bocar Thiam Alhamisi alisema kuwa TikTok itarejeshwa tu ikiwa kampuni hiyo itatia saini makubaliano ya kuruhusu kuondolewa kwa akaunti zinazoendeleza kile alichokitaja kuwa maudhui ya uchochezi.
“Kwa sasa, marafuku hiyo inadumishwa hadi kukamilika kwa makubaliano ya maandishi,” Bw Thiam alisema, kufuatia majadiliano na wawakilishi wa kampuni hiyo.
Marufuku ya TikTok ilifuatia kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko.
Mamlaka zilidai kuwa programu hiyo ilikuwa ikitumiwa kueneza “ujumbe wa chuki na upotoshaji” ambao ulitishia uthabiti wa nchi huku maandamano ya vurugu yakizuka kufuatia kukamatwa kwa Bw Sonko.
Serikali pia imeitaka TikTok kukubali kutoa fidia kwa watengenezaji maudhui wa Senegal ili warejeshwe.