Korea Kusini na Japan zimeripoti kuwa Korea Kaskazini imerusha makombora ya masafa marefu, katika ukiukaji wa maamzimio ya barala la Umoja wa Mataifa.
Jeshi la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini imerusha makombora kadhaa ya masafa marefu ambayo hayakubainika kuelekea Bahari ya Mashariki, inayojulikana pia kama Bahari ya Japan. Taarifa hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap, ambalo limenukuu kamandi kuu ya Jeshi la nchi hiyo, JCS.
Kikosi cha ulinzi wa pwani cha Japan, kimesema alau kombora moja linaaminika kuangukia baharini, kikinukuu taarifa iliyotolewa na wizara ya ulinzi. Korea Kaskazini ilipigwa marufuku na maazimio ya Umoja wa Mataifa kufyatua au hata kujaribisha makombora ya masafa yoyote.
Mzozo umeongezeka tena kwenye Rasi ya Korea katika miezi ya karibuni, hali iliyoisukuma Korea Kusini kusitisha makubaliano ya kijeshi na Kaskazini ya mwaka 2018, kuhusu hatua ya kujenga kuaminiana mpakani. Hatua hii ilifungua njia ya kurejea kwa luteka za kijeshi karibu na msitari wa mpaka wa kijeshi.