Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa Oktoba 17, 2023 aliongoza ujumbe wa Tanzania katika ufunguzi wa Mkutano wa Madini Muhimu na Mkakati kwa mwaka 2023 unaofanyika katika Jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini.
Mkutano huo unahudhuriwa na Viongozi, Watalaam, Taasisi za Fedha, Watengenezaji wa vifaa vya kielektroniki na baadhi ya Wawaziri wa Nchi za Afrika ikiwemo Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Malawi, Tanzania na Sudan Kusini.
Aidha, leo Oktoba 18, 2023, Mkutano huo utaendelea ambapo Tanzania kupitia Naibu Waziri Dkt. Kiruswa ataeleza kuhusu fursa za Madini Muhimu na Mkakati zilizopo nchini pamoja na Sera ya ujenzi wa mitambo ya kuchakata madini hayo ndani ya nchi.
Katika mkutano huo, Dkt. Kiruswa ameambatana na watalaam kutoka wizarani ambao ni; Kamishna Msaidizi wa Madini Mhandisi Ally Samaje, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Wa Madini Tanzania (GST) – Notka Banteze pamoja na Mjiolojia Joseph Ngulumwa.