Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Januari Makamba amesema Serikali iko katika mchakato wa kubadilisha utaratibu mzima wa kutoa kazi kwa Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kwa kuzingatia zaidi watakaokidhi vigezo vya utekelezaji miradi kwa wakati na viwango.
Ameyasema hayo leo Januari 24, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini.
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi hiyo hivyo haiwezi kukubali kuona wananchi wakiendelea kulalamika kutokana na kucheleweshwa kwa miradi husika.
“Tuko katika mchakato wa kubadilisha kabisa namna nzima tunawapa kazi, namna nzima tunatathmini hizi kazi na mwishowe hatima yenu kama Wakandarasi wa miradi ya REA.”
Akieleza zaidi, Waziri amesema Wizara kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itafuata taratibu zote na kuhakikisha inawaengua ambao wanasababisha malalamiko.
Aidha, amesisitiza kuwa kwa wale ambao wana utekelezaji duni zaidi na hawabadiliki, Serikali siyo tu kwamba itawachukulia hatua za kimkataba lakini pia itawashtaki kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Contractors Registration Board) ili waondolewe katika orodha ya Wakandarasi wa Tanzania.
“Haiwezekani wewe umepewa kazi unaendelea nayo, labda ulipaswa kuwa umefikia asilimia 90 lakini uko asilimia 40 na mwenzako kafikia asilimia 90 inayotakiwa halafu mnaenda kwenye ushindani huku mkiwa mmepewa nafasi sawa ya kupata kazi nyingine,” amefafanua.
Waziri Makamba amesisitiza kuwa ni kwa sababu hiyo, utaratibu unabadilishwa na kwamba Mkandarasi akipewa kipande kidogo cha kazi, akikamilisha atapewa kipande kingine na siyo vinginevyo.
Kufuatia kusuasua kwa baadhi ya wakandarasi katika utekelezaji wa miradi, Waziri Makamba ametoa muda wa miezi miwili kuanzia sasa ili waitumie kurekebisha dosari na mapungufu yao ili wafikie kiwango kinachotakiwa.
“Kama ulikuwa umesuasua, uko nafasi za chini au ya mwisho, tumia muda huo wa miezi miwili kuchakarika ili ufike kwenye nafasi inayotakiwa,” ameelekeza.
Akifafanua zaidi, amesema baada ya mwezi mmoja tangu kutolewa kwa agizo, Serikali itafanya tathmini ili kuanza kubaini waliozingatia maelekezo na kufanya mabadiliko na baada ya miezi miwili wale watakaokuwa na utekelezaji duni watakuwa wamefungua wigo wa kutoka nje.
Pamoja na kutoa maelekezo hayo, Waziri ameweka bayana kuwa lengo la Serikali ni kuwapa fursa wakandarasi wazawa lakini akatoa angalizo endapo wakishindwa kutimiza vigezo, basi Serikali haitasita kuwapatia kazi hizo Wakandarasi wa kimataifa waliothibitika kufanya kazi nzuri katika nchi mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Waziri amewaagiza Wakandarasi wote wenye utekelezaji duni kuwasilisha REA, Mpango wa namna ya kushughulikia ucheleweshaji miradi uliotokea (Delay Recovery Program) ndani ya siku saba tangu kutolewa kwa maagizo husika.
Akizungumzia mikakati zaidi iliyochukuliwa na Wizara kwa kushirikiana na REA katika kuhakikisha miradi ya umeme vijijini inatekelezwa kwa wakati, Waziri Makamba amesema mchakato wa kuajiri vijana 136 kwa kazi ya kusimamia miradi ya REA nchi nzima uko katika hatua za mwisho kwani usaili umekwishafanyika na hivi karibuni wataanza kazi.
Aidha, amebainisha kuwa, kunaandaliwa Jukwaa maalum kupitia tovuti (Website Portal) litakalotumika kuhuisha taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini ili kila mwananchi atakayeingia humo aweze kuona kwa uwazi hali halisi, wapi kunaendelea vizuri na wapi kunasuasua ili waweze kuhoji.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy amewakaribisha Wakandarasi wenye kuhitaji mazungumzo au msaada wowote kutoka REA, hususan waliokamilisha taratibu na wakawa na changamoto za kutokulipwa kwa wakati, wafike ofisini kwake, ambapo ameahidi kuzitatua.
“Niwahakikishie tu kwamba sisi REA tumeshakubaliana na kuweka mikakati ya dhati kwamba hatutachelewesha malipo kwa Wakandarasi kwani tunatambua umuhimu wa miradi hiyo kwa wananchi,” amesisitiza Mhandisi Saidy.
Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wenzake wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Styden Rwebangira amesema ni faida zaidi kwa Wakandarasi kupata fursa ya kuelezwa bayana mipango na hatua ambazo Serikali inakwenda kuzichukua dhidi ya wale wenye utekelezaji hafifu.
Amesema Serikali ingeweza isiweke bayana na kuchukua hatua kimyakimya hali ambayo ingewaathiri kwani wasingepata fursa ya kujirekebisha kama waliyopewa sasa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Namis Corporate, Mhandisi Thomas Uiso, akizungumza kwa niaba ya Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, amesema wamepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na watayafanyia kazi maana wanataka kuendelea kudumu katika kazi hizo.
“Nikuhakikishie Mheshimiwa waziri, katika wale watano wa juu kwa utekelezaji mzuri wa miradi, baada ya miezi miwili idadi itabadilika kabisa,” amesisitiza.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu ameitaja kampuni ya M/s STEG International Limited kufanya kazi nzuri kwani Mkandarasi huyo amekamilisha ujenzi wa miundombinu yote ya mradi kwa asilimia 100 kabla ya muda wa mradi kukamilika.
Amesema kazi aliyokamilisha Mkandarasi huyo ni kwa fungu (lot) 30 katika wilaya za Meatu na Maswa mkoani Simiyu na fungu 18 katika Wilaya ya Morogoro Vijijini mkoani Morogoro.
Mhandisi Olotu ameongeza kuwa ili kuhakikisha wananchi wengi wanaunganishwa na huduma ya umeme, Wakala umeongeza wigo wa njia za msongo mdogo (LV lines) kwa kilomita 2 pamoja na wateja 42 kwa kila kijiji.
Mkandarasi M/s STEG na wengine wawili kutoka kampuni za SAGEM COM Company Ltd na China Railway & Electrification Bureau wamepewa mkono wa pongezi na Mheshimiwa Waziri na watapatiwa zawadi maalum kutoka REA kutambua utendaji kazi wao mzuri katika kutekeleza miradi ya umeme vijijini.
Wakandarasi hao wameongoza kwa kushika nafasi nne za juu katika utekelezaji miradi.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wataalamu kutoka REA, TANESCO na Wizarani.