Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuingilia kati na kudhibiti kupanda kwa kasi isiyo ya kawaida kwa bei ya mbolea nchini.
Akizungumza na viongozi na wanachama wa jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma Desemba 22, 2021, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema iwapo serikali haitachukua hatua za muda mfupi, wa kati na mrefu kwenye suala la mbolea, wakulima wa Tanzania wataathirika sana.
Akipokea kero mbalimbali kutoka kwa wanachama na viongozi, Ado alielezwa kuwa bei ya mbolea imepanda kwa kasi Songea.
Mfano, mbolea aina ya Urea iliyouzwa Sh 52,000 msimu uliopita, sasa inauzwa Sh 105,000 kwa mfuko hali inayowafanya wakulima kushindwa kumudu kununua nakwmaba hali ipo hivyohivyo kwenye aina zote za mbolea.
Ado amesema kuwa ACT Wazalendo haijaridhishwa na majibu ambayo Waziri wa Kilimo Dk. Adolf Mkenda na Naibu wake, Hussein Bashe ambayo wameyatoa kuhusiana na suala la mbolea.
“Ndugu yangu Bashe alifika hapa Songea, akazungumza na wadau wa kilimo. Dk. Mkenda alifika pia, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mbolea duniani. Hawakuja na majawabu, walikuja na malalamiko. Kwamba bei ya soko la dunia na ugonjwa wa Korona ndio vimesababisha kupanda kwa bei ya mbolea. Hakuna hatua za maana za dharura walizosema,” amesema Ado na kuongeza;
“Tunatoa rai kwa Rais Samia Suluhu Hassan, aingilie upesi suala la mbolea na kuchukua hatua za upesi. Mosi, Serikali itoe ruzuku ili kushusha bei ya mbolea. Sehemu ya fedha za mkopo wa Korona kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) itumike kugharamia hili.
“Pili, katika msimu huu wa kilimo, Serikali ipunguze au iondoshe ushuru wa kuagiza mbolea nje ili kushusha bei. Tatu, katika hatua za muda mrefu, Serikali iwe na mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa mbolea nchini.
“Hivi sasa, viwanda vya ndani vinazalisha asilimia 5 tu ya mahitaji ya ndani. Kwenye Mkakati huo, Serikali iweke vichocheo (incentives) vya kuwavutia wawekezaji kwenye sekta ya viwanda vya mbolea,” amesema Ado.