Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuongeza ushiriki wa wananchi katika kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza kipato kwa wananchi wengi na kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na vijijini.
Majaliwa ameyasema hayo Mei 23, 2024 kwenye ufunguzi wa Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji baina ya Uganda na Tanzania, jijini, Dar-es-Salaam.
Amesema Serikali imeimarisha utoaji huduma kwa kuunganisha mifumo ya kielektroniki 55 ya taasisi 50, pia sheria 13 zimeshafanyiwa marekebisho ili kupunguza au kuondoa kodi, ada na tozo na kupunguza au kuweka misamaha ya ushuru wa forodha.
Awali, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alisema wizara yao itaendelea kusimamia na kuratibu diplomasia ya uchumi kikamilifu na kwa uadilifu mkubwa ikiwa ni kutimiza ndoto na azma za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Yoweri Kaguta Museveni za kukuza uchumi wa Tanzania na Uganda.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Wizara ya Mambo ya Nje (Masuala ya Kikanda) wa Uganda John Mulimba amesema kuwa Tanzania na Uganda ni nchi rafiki zinazoshirikiana katika maeneo mengi yakiwemo ya kibiashara, kiusalama, kielimu, hivyo undugu huo ni chachu ya maendeleo kati ya nchi hizo mbili ambao utasaidia kukuza uchumi wa wananchi wake kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Gilead Teri, amesema kongamano hilo limewakutanisha wawekezaji kutoka Tanzania na Uganda ili Kkufanya mambo kadhaa ya kiuwekezaji ikiwemo kubadilisha ujuzi.