Serikali imekamilisha mradi wa maji katika Kijiji cha Migongo Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma na kuwaondolea wananchi adha kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo waliyokuwa wakikabili tangu kupata uhuru.
Mradi huo wenye thamani ya shiling bilioni 1.1 hadi sasa umefikia asilimia 98 na kuzinduliwa na Waziri wa Maji Jumaa Aweso ambapo wananchi Elfu kumi na nne wameanza kufaidika na upatikanaji wa maji safi na salama.
Mwaka 2022 matumaini mapya ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Kijiji cha Migongo yalianza baada ya utekelezaji wa mradi wa maji kuanza na sasa Waziri Jumaa Aweso ameuzindua.
Kwa miaka yote walilazimika kutembea umbali mrefu na hata kupanda milima kutafuta huduma hiyo muhimu lakini bado kiu yao ilikuwa ni kuona mradi wa maji unafika katika eneo lao.
Baada ya uzinduzi wa mradi katika Mkutano na wananchi Waziri wa Maji Jumaa Aweso anatoa angalizo kwa kamati ya mradi huo ,kukusanya ankara za maji na kutumia fedha hizo kuendeleza mradi na sio matumizi binafsi.
Katika wilaya ya kasulu Mradi wa maji unaogharimu shilingi bilioni 1.2 kwa ufadhili wa shirika la Water Mission nao umezinduliwa na kutarajiwa kunufaisha karibu wakazi elfu 62 wa Vijiji vitatu vya kata ya Makere ambao walikuwa wakikabiliwa na adha hiyo.