Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesema Serikali imepiga hatua katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira licha ya changamoto zinazojitokeza.
Ameyasema hayo Desemba 18, 2024 alipokuwa kwenye ziara ya kikazi Zanzibar na kuongeza kuwa ushirikiano wa viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais umeleta tija katika sekta ya mazingira.
“Nina siku chache tangu nimeingia katika wizara hii lakini najiona mtu mwenye bahati kwani kwa muda mfupi tangu nimekuja nimejifunza vitu vingi kama nimekaa miaka miwili na hii inatokana na kuwepo kwa timu nzuri kwani ni watu wenye kasi katika utendaji wao wa kazi,” amesema.
Mhandisi Masauni amesema ingawa suala la mazingira si la Muungano linapokuja suala la uwakilishi, wananchi wa Zanzibar wanalitegemea kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuweza kupata fursa mbalimbali hivyo mipango thabiti inahitajika kwa maslahi ya nchi.
Aidha, kuhusu Uchumi wa Buluu Mhe. Masauni amesema ushirikiano utaendelea baini ya pande zote mbili kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kufungua zaidi milango ya uwekezaji katika eneo hilo.
“Mafanikio ambayo yanaonekana kwenye eneo la Uchumi wa Buluu ni ishara tosha kwamba tumeanza kupiga hatua hivyo tutaendelea kuliboresha na zile changamoto ambazo zimejitokeza kwa pamoja tunaendelea kuzipatia ufumbuzi,” amesema Mhe. Masauni.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya jitihada mbalimbali katika eneo hilo ikiwemo upatikanaji wa fedha kwa njia mbalimbali hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutoa ushirikiano ili kufanya eneo hilo kupiga hatua zaidi.