Serikali imesema hakuna uhaba wa Sukari nchini na kwamba upungufu uliopo hivi Sasa kwa mikoa ya kaskazini unatokana kiwanda cha TPC cha Moshi mkoani Kiilimanjaro kupunguza uzalishaji na Manyara Sugar cha mkoani Manyara kusitisha uzalishaji kutokanana ukosefu wa mali ghafi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji wakati akiwa kwenye ziara ya kutembelea kiwanda cha Sukari cha Manyara Sugar kilichopo kijiji cha Matufa Wilayani Babati ambacho kimesitisha uzalishaji kutokanana ukosefu wa mali ghafi.
Kauli hiyo ya Waziri Kijaji inakuja wakati huu ambapo Sukari imeadimika mitaani ambapo kilo moja ya Sukari iliyokuwa inauzwa shilingi 3,200 kwa rejareja katika miji ya Babati na Karatu Sasa inauzwa kati ya shilingi 3,800 hadi 4000, hali ambayo Wananchi wanaomba Serikali ifuatilie na kutafuta ufumbuzi.
Afisa uhusiano Kiwanda cha Manyara Sugar John Jeu amesema wamesitisha uzalishaji kwa sababu ya ukosefu wa malighafi za kutengenezea sukari.