Serikali imetoa wiki tatu kwa Mkandarasi wa kampuni ya China National Aero-Technology International Engineering Corporation (AVIC), anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Isyonje – Kitondo – Makete na sehemu ya Kitulo – Iniho yenye urefu wa kilometa 36.3, kwa kiwango cha lami, kufikisha vifaa na wataalamu, katika eneo la mradi, ili kazi ifanyike kwa haraka.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe.Innocent Bashungwa, akiwa wilayani Makete, mkoani Njombe, katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo ambao upo nyuma kwa mujibu wa mkataba, ambapo ameahidi kuwashughulikia wakandarasi wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi.
Aidha, Mhe.Bashungwa ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kumsimamia Mkandarasi huyo kwa karibu na kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana.